KISWAHILI UMEKOSA NENO MOJA TUUUUUUUUUUUUU!!!!!!!!

KISWAHILI; UMEKOSA NENO MOJA TU……

“Mwanadamu aliye uchi ni kiumbe mnyonge kuliko wanyama wote. Hana ngozi wala manyoya ya kumsitiri na nguvu za mazingira. Hana nguvu za simba wala mbio za swala, hana makucha ya chui, pembe za fahali au mbawa za tai. Licha ya unyonge huu, mwanadamu ni kiumbe pekee mwenye uwezo wa kubadili mazingira yake. Nyenzo pekee inayomwezesha kufanikiwa ni lugha”
Mawazo hayo yaliandikwa na waandishi Heese na Lawton kama utangulizi wao katika jitihada zao za kufafanua dhana ya lugha, nami sina budi kuyaazima kama katika utangulizi wangu katika makala haya. Uzuri wa lugha, umuhimu wake kwa mwanadamu na uwezo wake wa kusetiri utamaduni na kuurithisha toka kizazi kimoja kwenda kingine ni mambo ambayo yamejadiliwa kwa kina na watu mbalimbali na pasi na shaka iwayo yote wengi wetu tunakubali kwa hakika kwamba lugha ni nyenzo muhimu sana kwa mwanadamu. Hivyo sioni kama ni busara sana kuzijadili dhana hizo tena bali nijikite katika kiini hasa cha makala haya.
Lugha yetu ya Kiswahili imepungukiwa na jambo moja, likifanyika hilo itavuka vizingiti vyote vinavyoikingama na kutamalaki katika mawanda mapana kuliko ilivyo hivi sasa. Kabla ya kulitaja jambo hilo niwakumbushe wasomaji kisa kimoja kilichoandikwa katika Biblia. Kwa wasomaji wa Biblia hawatakuwa wamekosa kusoma simulizi moja maarufu lililorekodiwa katika kitabu cha Marko juu ya mtu mmoja tajiri aliyetamani kuurithi uzima wa milele. Katika kisa hicho mtu huyo alimwendea Yesu na kumwuuliza ni jambo gani afanye ili akaurithi uzima wa milele. Yesu, tunaambiwa, alimwangalia mtu huyo na kumtajia amri kumi za Mungu anazo takiwa kutimiza. Yule mtu kwakujiamini akajibu kwamba amri hizo amezitimiza tangu akiwa motto
Yesu, tunaambiwa, alimkazia macho akampenda na kumwambia “Umepungukiwa na neno moja. Enenda ukauze ulivyonavyo vyote, uwape maskini,….kisha njoo unifuate”. Tunaelezwa ya kwamba mtu huyo alikunja uso na kuondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi. (Marko 10: 17-22)
Tukirudi katika lugha yetu ya Kiswahili, tumeshuhudia mijadala isiyo na ukomo juu ya uwezo wa lugha hii katika utumizi wake hasa uwezo wake katika kutolea elimu kwenye shule za sekondari hadi elimu ya juu. Midahalo mingi imefanyika tangu katika ngazi ya wanafunzi wa sekondari hadi kwa wanazuoni waliobobea. Suala hasa limekuwa ni kama lugha ya Kiswahili inaweza kufundishia masomo hasa ya sayansi na kama inaweza kuhimili kasi ya utandawazi.
Binafsi naungana na wale wote wanaokiona Kiswahili kuwa kinaweza kumudu na kukabiliana na changamoto zote zinazotolewa lakini hili linategemea jambo moja kubwa. Jambo hilo ni nguvu ya uongozi na hasa uongozi wa juu serikalini. Ili kuipa mashiko, hoja hii tujaribu kuidurusu historia ya Kiswahili kwa kuangalia mambo machache.
Kiswahili kilifanywa lugha rasmi ya kutumika mashuleni na katika shughuli za kiserikali na watawala. Kilifadhiliwa na kufanyiwa utafiti, usanifu, na kuundiwa sarufi na watawala. Mbali na wakoloni wa Kijerumani kuanza kukitumia katika shughuli zao rasmi za kiserikali, Waingereza walifanya kazi kubwa zaidi ya kukipa misingi imara. Hoja yangu hapa ni kwamba si umma uliolazimisha Kiswahili kiwe lugha rasmi bali ni utawala. Nguvu kubwa ya kukieneza na kukisambaza Kiswahili ilifanywa na watawala.

Kwa waliopata kusoma vitabu vingi vya Kiswahili vilivyochapishwa baada ya robo ya kwanza ya karne ya ishirini hawatakosa kumkumbuka Hayati Frederick Johnson aliyekuwa katibu mkuu wa kwanza wa Kamati ya Fasihi ya Afrika ya Mashariki (East African Literature Committee). Bwana Johnson aliweza kufasiri katika lugha ya Kiswahili vitabu kama Mashimo ya Mfalme Suleiman, Saafari za Gulliver, Hadithi ya Alain Quitermain, Mazungumzo ya Alfu-lela-u Lela, Kisiwa chenye Hazina na vingine vingi.
Ikumbukwe pia kwamba vitabu vya kufundishia mashuleni kwa wakati huo kama vile Milango ya Historian a vingine vingi vilivyoandikwa na wazawa katika lugha ya Kiswahili vilipewa msukumo na utawala ili Kiswahili kiweze kuwa na mizizi imara. Ijapokuwa watawala hao watakuwa walikieneza Kiswahili kwa maslahi yao ya kiutawala, hili haliondoi ukweli kwamba wao ndio waliokieneza Kiswahili kwa kiasi kikubwa na kukisanifisha katika lahaja maalumu.
Tukijaribu pia kuangalia wakati na baada ya uhuru, juhudi za utawala katika kueneza na kuimarisha Kiswahili ziko dhahiri. Ni nguvu ya utawala iliyopitisha lugha ya Kiswahili iwe rasmi katika Tanganyika huru. Ni nguvu ya utawala ilyopitisha lugha ya Kiswahili itumike kama lugha ya kufundishia masomo karibu yote katika shule za msingi.
Rais wa kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere, mathalani, licha ya kuandika vitabu mbalimbali katika lugha ya Kiswahili, alihimiza pia matumizi ya lugha hii kwa kupitia kauli mbiu mbalimbali. Harakati za Kisomo cha Watu Wazima zaweza kuwa mfano dhahiri katika kuthibitisha hili. Tanzania, nchi maskini na iliyoingia vitani na Uganda mwishoni mwa miaka ya sabini, bado iliweza kufanya vema wakati huo katika kufuta ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika.
Haya yaliwezekana si kwa sababu ya fedha au uchumi uliostawi bali ni kwa utashi wa uongozi wa juu uliokuwa madarakani na moyo wa wananchi katika kuitikia wito kwa uongozi wao. Hadithi za Bwana Matata zilipamba moto katika kila kona ya nchi yetu hasa hasa katika mazingira ya vijijini. Kauli mbiu ya Mwalimu Nyere iliyosema “Wakati ni huu!” ikiwahimiza watu wazima kujikomboa kutoka katika makucha ya kutojua kusoma na kuandika. Haya yote yalichangia kwa kiasi kikubwa katika kukua na kuenea kwa Kiswahili.
Walimu waliosaidia harakati hizi wengi wao walikuwa wanajitolea. Madarasa yalikuwa nyumba za mabalozi wa nyumba kumi kumi. Nakumbuka vijana wahitimu wa daras la saba kwa wakati huo waliokusanyika nyumbani kwetu kusaidiana na baadhi ya walimu kufundisha madarasa ya watu wazima waliokuwa wanajifunza kusoma na kuandika Kiswahili kw a bidii.
Naikumbuka misemo kama, “Ndizi huleta pesa pyai” badala ya “Ndizi huleta pesa pia” na msemo “Ndizi ni kyakulya” badala ya “Ndizi ni chakula”. Hiyo ni baadhi ya misemo iliyowasumbua bibiu na babu zetu katika jitihada zao za kujifunza Kiswahili. Nayakumbuka haya yote kadiri ninavyozidi kuitafakari nguvu ya kushawishi na kuvuta umma aliyonayo kiongozi anapoamua kuwaelekeza watu katika jambo fulani.




Faida ya jitihada hizo inaonekana hadi leo. Popote Tanzania waweza kwenda na kuwasiliana na watanzania wenzako katika lugha ya Kiswahili bila ya matatizo yoyote. Iwe katika biashara, kazi au majukumu mengine ya kimaisha. Kwa sasa inashangaza kuona kwamba baada ya zaidi ya robo karne tangu wakati huo, tunadai kwamba lugha ya Kiswahili haiwezi kukabiliana na vikwazo vya utandawazi. Katika zama ambazo tuna idadi kubwa zaidi ya wasomi na taasisi za kutolea elimu kulinganisha na wakati huo.
Ni hapo ninapojenga hoja kwamba uongozi wetu na hasa uongozi wa juu ungetia shime katika kukinadi Kiswahili na hayo yanayoonekana kuwa vikwazo, umma ungefuata nyuma na kukabiliana na changamoto hizo. Tanzania ina wasomi wengi wanaofundisha katika taasisi mbalimbali za nje ya nchi. Tusishangae kuwasikia wasomi hawa wa kitanzania wakifasiri na kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi za Ujerumani, Uingereza, Marekani, Botswana, Afrika ya Kusini na kwingineko nje ya nchi yao wakati hapa nyumbani tukikikebehi Kiswahili hichohicho kwamba hakiwezi kukabiliana na vikwazo vya utandawazi.
Nakumbuka mwezi Machi mwaka 2004, Profesa Hamis akitoa mada katika kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria mkoani Kagera, aliwaambia wanafunzi hao kwamba alikuwa katika hatua za mwishomwisho katika kukamilisha kazi ya kuandika kamusi ya Kiswahili-Kiarabu. Kazi ambayo alikuwa amepewa na serikali ya Sudan. Huyu ni msomi mtanzania na anaishi Tanzania. Nchi jirani zinaiona hazina tuliyonayo na kuitumia huku sisi tukilumbana kama Kiswahili kinafaa au hakifai. Sitarajii wanazuoni kama hawa wanashindwa kukisaidia Kiswahili kukabiliana na changamoto zinazokikingama.
Shirika moja la dini la Mashahidi wa Yehova lenye makao yake makuu huko Brooklyn, New York nchini Marekani huandika machapisho yake mengi katika lugha mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kiswahili. Mathalani katika magazeti yake yajulikanayo kama Mnara wa Mlinzi na Amkeni, huandika mbali na mambo yanayohusu imani yao, makala mbalimbali za kitiba, kisayansi kijiografia na kijamii kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa umahili mkubwa. Iwapo watu hawa huko Marekani wanaweza kukitumia Kiswahili katika kufafanua mambo yote haya iweje sisi wazawa, wenye lugha, tushindwe?
Tujaribu kukumbuka maeneo machache ambako nguvu kidogo ya viongozi katika kushawishi na kuelekeza imeweza kuleta athari inayoonekana upesi. Mathalani katika uongozi wa awamu ya pili wakati timu ya soka ya taifa ilipokuwa inafanya vibaya katika michezo yake, raisi wa wakati huo aliwahi kutoa kauli kwamba timu hiyo ni sawa na kichwa cha mwendawazimu. Kauli hiyo ilipata nguvu, ikanukuliwa na vyombo vya habari na ilidumu kusemwa na kurejewa na watanzania wengi. Hoja hapa ni kwamba, huo haukuwa msemo mpya katika lugha bali uzito wa kauli hiyo ulitokana na uzito wa mhusika aliyeitoa.
Tukiangalia mwamko uliopo kuelekea timu ya taifa ya soka ya sasa, hakuna shaka kwamba ni pamoja na jitihada binafsi za mheshimiwa rais wan chi. Watanzania wengi wamehamasika, wameweza kununua na kuvaa jezi za timu yao ya taifa, wanaishangilia na kuipenda. Sio siri kwamba hamasa hii kwa kiasi kikubwa ni pamoja na kumwona kiongozi wao wan chi akijumuika nao katika kuiunga mkono timu hiyo. Wabunge wamefuata mkondo huohuo na imeweza hata kuzungumzwa katika mojawapo ya hotuba rasmi za mheshimiwa rais.

Ni kwa mtazamo huo basi nashawishika kuamini kwamba Kiswahili kimetimiza yote, na kimeyatimiza tangu zamani, lakini kimekosa neno moja tu., nalo ni msukumo wa dhati kutoka katika uongozi wa juu wa nchi. Hili likifanyika, mengine yote yatawezekana.

Naomba kutoa hoja.

Johansen Kempanju
jkempanju@yahoo.com
0713 507203
Mwanafunzi, Shahada ya Kwanza ya Elimu (B.Ed)
Chuo Kikuu cha Tumaini
Chuo Kikuu Kishiriki-Makumira
Arusha.



















































































Meshack Maganga
2009
Previous
Next Post »

MAONI ConversionConversion EmoticonEmoticon