TAFSRI ZETU ZA BIBLIA

" Tafsri Zetu za Biblia" zinatupeleka wapi?
Biblia ni neno lenye asili ya Kiyunani bi.bli`a ambalo humaanisha vitabu vidogo. Ni mkusanyiko wa jumla ya vitabu 66 ambavyo kwa pamoja huitwa Biblia na ni vitabu hivi ambavyo kwa ujumla wake, kulingana na imani ya wakristo, hufanyiza kitabu kimoja kitakatifu.

Ni neno la Mungu ambalo kwa imani Mungu aliwaongoza wanadamu mbalimbali kuliandika kwa muda wa takribani miaka 1,600 kuanzia wakati Misri likiwa taifa lenye nguvu sana ulimwenguni chini ya utawala wa mafarao kabla ya Yesu Kristo hadi wakati Rumi ikiwa miliki yenye nguvu ulimwenguni baada ya Yesu Kristo. Kulingana na Guinness Book of World Records, {1988} inakadiriwa kwamba naskala za Biblia zaidi ya bilioni mbili na nusu zilikuwa zimechapishwa kati ya mwaka 1815 na 1975. Ni kitabu kilichopata changamoto kubwa katika hisoria ya maandishi labda kuliko kitabu chochote kile. Kimetafsrwa katika lugha nyingi sana, kimepigwa marufuku katika sehemu mbalimbali na hata kuchomwa moto katika maeneo kadha wa kadha lakini bado kimeendelea kuwepo na nakala zake zinazidi kuongezeka.
Ni kitabu ambacho hakikuwa kimegawanywa katika sura na mistari kama kilivvyo sasa hadi karne ya 16 pale Robert Estienne {Stephanus} aliyekuwa mhariri mashuhuri huko Paris Ufaransa alipoianza kazi hiyo ili wasomaji waweze kufanya marejeo kwa urahisi kwa kuongozwa na sura na mistari husika.
Usahihi wa Biblia bado ni changamoto kwa baadhi ya watu na ni mjadala ambao hautaisha kwani ni msukumo wa imani ya mtu binafsi juu ya kile kilichoandikwa humo, lakini hoja yangu si juu ya hilo wala juu ya historia ya Biblia, bali ni juu ya tafsri zinazotolewa na wakristo mbalimbali katika madhehebu yao. Tujaribu kurejea matukio ya hivi karibuni yanayofanywa na wakrito kwa kutegemea tafsri zao za neno la Mungu katika Biblia. Wengi tunamkumbuka Kibwetere wa Uganda ambaye kwa kutumia Biblia aliwakusanya wakristo na kuwaandaa katika kanisa lake ili wampokee Yesu anaporudi katika tarehe aliyoifahamu Kibwetere mwenyewe. Siku ilpowadia aliwachoma moto hadi kufa baada ya kuhakikisha kwamba wameuza kila walichokuwa nacho na kumkabidhi fedha zote. Hapa Tanzania uliripotiwa mgogoro katika baadhi baadhi ya vyombo vya hababari kuwa katika baadhi ya shule za msingi huko Mbeya mnamo Setemba 2007 wanafunzi walikataa kutii bendera na wimbo wa taifa hadi ikapelekea waziri wa elimu kwa wakati huo, Magreth Sitta, kuingilia kati. Hao pia ni wakristo waliojenga msimamo wao kwa kutegemea tafsri zao za Biblia.
Mwanzoni mwa mwaka huu, mkristo mwingine huko Mbeya alilipotiwa na vyombo vya habari kuwa aliwaongoza wenzake kwenda kuweka kambi porini kuisubiri siku ya mwisho. Jambo ambalo serikali iliamua kuingilia kati na kusitisha zoezi hilo.
Hao pia walitegemea tafsiri zao za Biblia. Tangu mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu, wakristo Waadventista Wasabato Masalia wamekuwa wakienda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam wakitaka kwenda nchi za ng`ambo kuhubiri injili bila ya kuwa na tiketi wala vibali vya kuwaruhusu kusafiri kwenda katika nchi husika na mara zote wamefukuzwa toka uwanjani hapo. Wanakiri, katika mahojiano na vyombo vya habari, kwamba hawana hata uelewa wa lugha inayotumika katika nchi wanazokusudia kwenda kuhubiri, lakini kwa kutegemea tafsiri wanazozifanya katika vifungu vya Biblia, wanaamini kwamba watasafiri kwa ndege na kuhubiri huko bila vibali, tiketi wala kujua lugha husika! Tukijaribu kuangalia kuibuka kwa utitiri wa madhehebu kila kukicha huku kila kiongozi wa dhehebu jipya akijinadi kukidhi mapungufu yanayojitokeza katika madhehebu yaliyomtangulia..
Wote hawa wanatafsiri vifungu mbalimbali kutoka katika Biblia. Kwa sasa si jambo la ajabu kukuta nyumba za ibada katika vchochoro vya ajabu ajabu; nyumba ya kawaida iliyozungukwa na mabaa kila upande na kumbi za starehe inakuwa kanisa lililoanzishwa na mkristo anayejitangaza kuwa mchungaji wa dhehebu fulani jipya.
Mchungaji huyu na wafuasi wake kila mara wakati wa ibada wanashindana kupaza sauti kati yao na muzik kutoa baa na kumbi za starehe zilizowazunguka! Madhehebu yanaendelea kuanzishwa ndani ya madhehebu, waumini ndani ya dhehebu moja wanakuwa wachungaji na kuanzisha madhehebu mapya. Wananyag`anyana waumini na matokeo yake mshikamano miongoni mwa waumini, aliouhimiza Yesu Kristo, unazidi kutoweka.
Kikatiba nchi yetu imetoa uhuru wa kuabudu kwa kila mmoja, hivyo si haki mtu mmoja kuingilia uhuru wa mtu mwingine. Kwa kutambua hilo naandika makala haya kutokana na ushawishi wa mitazamo ya wakristo wenzangu na wala si katika kuingilia uhuru wao katika kuabudu. Mathalani, kijana Daniel Masinde {16}, mmojawapo wa Waadventista Wasabato Masalia wanaotaka kwenda nchi za ng`ambo kuhubiri injili bila tiketi wala vibali, alinukuliwa na gazeti moja litolewalo kila siku akidai kwamba amemaliza elimu ya msingi huko wilayani Bunda mkoani Mara mwaka jana na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari lakini hakuona umuhimu wa elimu ili kwanza akamtumikie Mungu. Jenifa Masinde {18}, dada yake na Daniel, naye alinukuliwa akidai kuwa yupo kidato cha tatu katika shule ya sekondari Elizi iliyoko mkoani Mara lakini ameamua kuacha shule na kujiunga na wakristo wenzake wakisubiri kwenda kimiujiza kueneza injili barani Asia. Vijana hawa wanadai kwamba uamuzi wao huo unapongezwa na viongozi wao pamoja na wazazi wao! Msimamo na mtazamo wao unategemea tafsri zao katika vifungu vya Biblia.
Lakini Biblia hiyo hiyo inasisitizajuu ya umuhimu wa elimu na manufaa yake. Biblia ambayo wengi wa waandishi wake mbali na kuongozwa na Mungu walikuwa wasomi na waliweza kuandika kwa mikono yao wenyewe.
Tuchukulie kwa mfano Musa, mwandishi wa vitabu vitano vya kwanza katika Biblia, Kitabu cha Ayubu pamoja na sehemu ya Zaburi; anatajwa kuwa msomi mzuri mbali ya kuwa nabii na kiongozi. Pia Luka, mwandishi wa Injili ya Luka na kitabu cha Matendo ya Mitume, anatajwa kuwa msomi na tabibu mzuri, Paulo anadhihirisha usomi wake kwa nyaraka nyingi alizoziandika, hao ni kwa kutaja wachache. Wengi wa watumishi wa Mungu waliitafuta elimu na Mungu akawatumia kwa manufaa pamoja na elimu yao.
Iangalie sura ya Biblia ya sasa, Mungu amewawezesha watumishi wake wenye elimu kufanya kazi ya kuipa muundo ilio nao leo hata Daniel na Jenifa wakaweza kuisoma. Tujiulize juu ya lile agizo katika Biblia kwamba ni wajibu wa kila mmoja wetu kufanya kazi {Wathesalonike 4:11} Itakuwaje basi tusipojifunza maarifa na ujuzi mbalimbali wa kutuwezesha kufanya kazi? Ni ipi nia ya viongozi wa dini wanaowashawishi wafuasi wao wasijiendeleze kielimu na kujishughulisha katika shughuli za kujikimu kimaisha? Yesu Kristo alisisitiza kwamba watu kutoka mataifa yote wawe wanafunzi {Mathayo 28:19} Kama manafunzi ni mtu anayejifunza, basi agizo hilo linatutaka tujifunze juu ya Yesu Kristo na Ufalme wa Mungu. Lakini linalofanyika sasa kwa wakristo tulio wengi ni kufanywa wafuasi wala si wanafunzi, tena tunafanywa wafuasi wa wanadamu wenzetu ambao kwa kutumia tafsiri zao katika vifungu vya Biblia wanageuka kina Kibwetere wapya. Bila shaka yanahitajika majaliwa ya Mungu ili kuweza kuyapambanua maneno yake.
Lakini ni lazima pia tujihadhari na watu mahiri wa kushawishi ambao kwa uwezo wao mkubwa wa kunukuu vifungu vya Biblia na kufanya tafsiri zao wanatimiza matakwa yao binafsi wakishawishi hiki kiwe hivi na kile kiwe vile.
Mwandishi wa kitabu cha Zaburi kwa kutambua hilo aliomba jambo moja ambalo hata sisi wakristo wa leo tunaweza kuliomba ili kuepuka kuwa wafuasi kwa wanadamu. Yeye aliomba afundishwe na Mungu mwenyewe ili aweze kutenda yanayostahili na aongozwe namna ya kuishi duniani kadiri inavyotakiwa {Zaburi 143:10} Nimeshuhudia muumini mmoja aliyejitenga na kanisa lake na kuanzisha kanisa jipya. Yeye amekuwa mchungaji na baada ya kupata wafuasi kiasi ameandaa siku maalum, "Siku ya Mke wa Mchungaji". Katika siku hiyo waumini wote wakina mama walitakiwa kuleta chochote kinachoweza kumfaa mke wa mchungaji. Siku ilpowadia walikusanya vyakula vya kila namna, nguo, fedha pamoja na zawadi za namna mbalimbali na kumpelekea Mama Mchungaji.
Waliombewa na kutakiwa kuondoka na baraka za Bwana wakati wengine kati yao wakiwa hawana hata uhakika wa kupata mlo wao wa jioni. Bado najiuliza kama mchungaji huyu ataandaa pia siku ya mtoto wa mchungaji au siku ya shemeji yake! Hayo ndiyo mazingira ya imani zinazoikabili jamii yetu. Baadhi ya waumini wanatakiwa kutoa hata kile kidogo walichonacho kumwongezea mwenye nacho ili wapate baraka za Mungu.

Tafakari
Johansen Kempanju
{mwanafunzi} Chuo Kikuu cha Tumaini-Arusha jkempanju@yahoo.com
0713 507203










Copyright Meshack Maganga 2009
Previous
Next Post »

MAONI ConversionConversion EmoticonEmoticon