USTARABU NA UTAMADUNI WA MAGAHARIBI

Manukato ya Ustaarabu na Utamaduni wa Magharibi katika Ukristo

Katika makala yangu fupi iliyochapishwa katika gazeti hili toleo namba 4057 na kurudiwa tena katika toleo namba 4085 chini ya kichwa Imani ya Kikristo ipo katika Kipindi cha Mpito? Nilibainisha mambo machache sana ambayo kwa asili yake ni utamaduni binafsi wa waenezaji wa imani ya Kikristo katika Afrika lakini yamechanganywa (kwa maksudi?) na Ukristo mpaka yakapokelewa na kuabudiwa na wakristo wa Afrika kama sehemu ya Ukristo.
Nilipokea jumbe nyingi za simu na barua pepe kutoka kwa wasomaji mbalimbali wakitoa ma oni tofauti tofauti juu ya makala hayo na wengi wakitaka kujibiwa kwa maswali niliyouliza katika makala hayo. Sikupenda kuandika tena juu ya imani kwani kama nilivyobainisha makala niliyotaja mwanzoni, nguvu ya imani ni kubwa kwa namna isiyopimika. Yaweza kumtia mtu yeyote upofu hata akajaribu kukanusha mambo yaliyodhahiri. Kwa hali hiyo basi, ujumbe niliopata kutoka kwa msomaji aliyejitambulisha kwa jina kama ndugu William Mauki umnisukuma kuchukua kalamu na kuandika makala haya. Kifupi ndugu Mauki anaona kwamba ni suala la uoga kujadili juu ya kile tunachokiamini na kutaka kurudia mila na desturi zetu (za kishenzi?) kama kuvaa majani badala ya nguo n.k
Kabla sijazungumzia maoni hayo, napenda kubainisha kwamba mmi ni mshiriki katika Imani ya Kikristo na siandiki dhidi ya Ukristo bali dhidi ya tamaduni zinazopingana na Ukristo lakini zimeambatanishwa nao na kuchukuliwa kama sehemu yake.

Ni kwa mtazamo huu naungana na waandishi Mvungi, M na Omari, C.K wanaposema kwmba " Ukristo ulipokuja mnamo karne ya 19 na Uislamu mapema zaidi ya hapo, mambo mengi ya mila za asili yalianza kubadilika. Kwa kiasi fulani, Uislamu kidogo uliweza kuvumilia mila na desturi za asili, lakini kwa Ukristo, kila kitu cha Mwafrika kilikuwa ni cha hali ya chini, cha mtu mshenzi." Urithi wa Utamaduni Wetu TPH 1981 Dar es Salaam uk 42.
Ni kwa misingi ya utamaduni na ustaarabu huu wa Magharibi kujumuishwa katika UKristo ninapojenga hoja yangu kwamba kujadili na kudadisi juu ya yale tunayoyaamini ni jambo sahihi na linalokubalika katika Ukristo. Ili tuweze kupambanua kati ya imani kwa Mungu kupitia Kristo Yesu na ustaarabu na utamaduni wa Magharibi kupitia wamishionari. Katika kuichunguza dhana hii, turejee baadhi ya maandiko katika Bibliaili tuone ni nini walichokifanya waamini wa kwanza walipopelekewa imani hii ngeni kwao. Waliyachunguza maandiko kila siku ili waweze kuwa na uhakika juu ya kile wanachoambiwa. (Matendo ya Mitume 17:10-11)
Nikirejea kwenye hoja ya ndugu yangu Mauki, namkumbusha kutofautisha kati ya mambo mawli; utamaduni wa mwafrika kuchanganywa na ule wa magharibi na imani katika Mungu kupitia Kristo Yesu kuchanganywa na utamaduni huo. Katika kuvaa, kula, kunywa na kuiga mambo mengine kutoka katika utamaduni huo si sawa kuchukulia mambo hayo kama sehemu ya Ukristo, imani ambayo inajisimamia na kutahadharisha juu ya kuchanganywa.
Ili kuitalii dhana hii kwa mapana kidogo, tujaribu kuchunguza mifano michache ifuatayo;
Nilizungumzia juu ya uvaaji wa nguo nyeusi katika misiba, dessturi ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa kuandaa keki na tukio la kuwasha na kuzima mishumaa katika sherehe hizo. Ni mambo ambayo tumeyazoea na tumeyaadhimisha tangu tukiwa watoto lakini ukiambiwa kwamba chanzo chake ni upagani labda unaweza usiamini. Labda kwa nyongeza tujiulize pia nafasi ya Father Christmas na sherehe za Krismasi katika Ukristo, tujaribu kujiuliza pia sisi kama wakristo tunapohangaika kutazama nyota zetu kwa siku (zodiac) kama kwa kufanya hivyo tunatimiza fungu la Ukristo.

Tukirejea katika sherehe ya siku ya kuzaliwa, Biblia inawataja watu wawili tu waliofanya 'Birth Day Party' ambao kama wewe ni msomaji wa Biblia hata kwa kuwataja majina yao utashtuka. Hao si wengine bali Farao wa Misri ambaye sikukuu yake ya kuzaliwa iliambatana na mauaji kwa kumtundika mtu na mwingine ni Herode ambaye naye pia aliamuru kuuawa kwa Yohana Mbatizaji katika sherehe yake ya kuzaliwa. (Mwanzo 40:20-22 na Marko 6:21-27). Hatajwi nabii yeyote au mtumishi wa Mungu aliyeadhimisha sikukuu yake ya kuzaliwa.
Waandishi Ralph na Adelin Linton katika kitabu chao The Lore of Birthdays (New York 1952) wanaeleza "Wagiriki waliamini kwamba kila mmoja alikuwa na roho au demon yenye kumlinda iliyohudhuria kuzaliwa kwake na kumlinda maishani. Roho hiyo ilikuwa na uhusiano wa kimafumbo pamoja na mungu ambaye katika ukumbusho wa siku yake ya kuzaliwa kwake mtu huyo alizaliwa". uk wa 8. Kwa mtazamo huo utaona kwamba desturi mbalimbali kama hizo zina historia ndefu. Yasemekana kwmba kutoa pongezi, zawadi na mishuma iliyowashwa zilikusudia kumkinga mwenye kuadhimisha ukumbusho wa siku yake ya kuzaliwa asiumizwe na mashetani na kuhakikisha usalama wake kwa ajili ya mwaka ujao.
Vipi kuhusu kutengeneza keki na kuwsha mishumaa juu ya keki hizo si namna ya ibada? Ralph na Adelin katika kitabu nilichokitaja hapo juu wanaeleza..."Desturi ya mishumaa ilyowashwa juu ya keki ilianzishwa na Wagiriki, keki za asali zenye mviringo kama mwezi na kuwashwa kwa mishumaa midogo yaliwekwa juu ya madhehebu ya hekalu la Artemi". uk 14. Ikumbukwe kwamba Artemi ni mungu-mke (godness) wa Wagiriki ambaye kwa Warumi anjulikana kama Diana ambaye alitumika katika shughuli za uwindaji na uzazi. Katika Ukristo , kuabudu miungu mingine tofauti na Mungu wa Israeli ni kinyume kabisa. (Kumbukumbu la Torati 5:6-10). sasa je, tunapofanya ibada ama kwa kujua au kutojua kuelekea miungu mingine tunatekeleza matakwa yw Ukristo?
Wakristo wa kwanza walitakiwa kufanya kila jambo kwa utukufu wa Mungu. (1Wakorintho 10:31). Sisi je, Hayo tunayoyafanya kwa kivuli cha Ukristo ni kwa utukufu wa nani? Tulikatazwa kumwabudu Mungu huyo huyo aliyejulikana kwetu kama Mlungu, Izuva, Iruwa, Katonda, Zuwa, Nguluvi, Engai na majina mengine mengi kulingana na lugha ya jamii husika kupitia kwa miungu kama Mugasha, Irungu, Wamala pamoja na wahenga wetu wengi waliolala.. Badala yake tukatakiwa kumwabudu Mungu huyo pamoja na miungu kama Artemi, Apolo na 'watakatifu' ambao kuwepo kwao hakutofautiani na kuwepo kwa wahenga wetu waliolala mauti.

Japo kuna mengi ya kuchunguza na kujihadhari nayo katika imani, ni jambo la kufurahisha kwamba jumuiya ya wakristo kupitia madhehebu yao wanajadili mambo mbalimbali yanayohusu imani yao kwa kiasi fulani ili wazidi kuimarika katika imani yao. Kwa sasa tunaweza kuona programu kama Bible Studies, Mafungo, vipindi vya maswali na majibu kupitia redio na televisheni n.k. Kwa mantiki hiyo udadisi unaoweza kuchochewa na makala haya miongoni mwa wasomaji, unaweza kuwaelekeza katika kutafuta majibu ya kuimarisha imani yao.

Mwanafunzi
Johansen Kempanju
Tumaini University
Makumira University College
Faculty of Humanities (B. Ed 1)
email:
jkempanju@yahoo.com
mobile: 0713 507203

Copyright Meshack Maganga 2009
Previous
Next Post »

MAONI ConversionConversion EmoticonEmoticon