Walimu wetu sasa wapigwe risasi?

Walimu wetu sasa wapigwe risasi?

Mojawapo ya watu waliotajwa sana katika karne iliyopita, bila shaka ni pamoja na Adolph Hitler. Huyu si mwingine bali ni yule mbabe wa kivita ambaye kwa kiasi kikubwa anawajibika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia ya mwaka 1939 hadi 1945. Huyu ni mtawala wa Ujerumani tangu Agosti 2 mwaka 1934 hadi April 30 1945. Tukiacha ukatili mkubwa anaotajwa kuufanya enzi za utawala wake, hasa dhidi ya Wayahudi aliowaua kwa mamilioni akitumia gesi za sumu, bado tunaambiwa na wanahistoria kwamba katika enzi za utawala wake aliiletea nchi yake ya Ujerumani maendeleo makubwa ambayo viashiria vyake vipo hadi leo..
Inasemekana kwamba katika utawala wake wa kiimla aliiwezesha Ujerumani kuwa na barabara pana na nzuri kwa kuwatumikisha Wajerumani usiku na mchana. Barabara hizo tunaambiwa zipo na zinatumika hadi leo. Tunaambiwa pia kwamba kwa amri zake na vitisho aliwawezesha wahandisi wa Kijerumani kuvumbua gari aina ya Volkswagen, gari ambalo lilikuwa na gharama nafuu sana. Wahandisi hao, tunaambiwa, walifungiwa na Hitler mwenyewe na kuwapa muda maalum akiwataka kwamba wakifunguliwa wawe na maelezo ya kutosha kumshawishi ni jinsi gani ya kutengenezaa gari litakaloweza kununuliwa na kila Mjerumani. Kukosekana kwa jibu la namna ya kutengeneza gari hilo ungekuwa mwisho wa maisha yao.
Hakuishia hapo, tunaambiwa hata timu ya soka iliweza kubeba kombe la dunia kwa amri na vitisho hivyohivyo. Wacheza waliambiwa kwamba wasipokuja na kombe wasirudi Ujerumani. Na kwa vitisho hivyo, tunaambiwa, waliweza kurudi na kombe nyumbani. Hayo pamoja na mengine mengi yalifanikiwa katika Ujerumani ya wakati huo si kwa sababu ya ubabe na mabavu aliyoyatumia Hitler tu, bali ni pamoja na mshikamano wa Wajerumani katika utendaji wa pamoja hata kama hili litakuwa lilifanyika kwa kulazimishwa. Naamini kwamba katika Ujerumani ya Hitler hakukuwa na tofauti kubwa ya kimaslahi kama ilivyo katika nchi yetu kwa sasa.

Ujerumani ya wakati huo nimeirejelea kwa kirefu kidogo baada ya kutafakari matokeo ya wanafunzi wa shule za msingi yaliyotolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hivi karibuni. Takwimu zinaonyesha kwamba kiwango cha kufaulu kimeshuka sana kwa mwaka huu, mbali na matarajio ya wengi kwamba kutokana na ongezeko la shule za sekondari, maarufu kama shule za kata, kiwango cha kufaulu cha watoto wa shule za msingi kingeongezeka ili kuendana na ongezeko la shule hizo. Kinyume chake, takwimu zilizotolewa na serikali kupitia kwa Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, zinaonyesha kwamba kati ya wanafunzi 999,070 waliofanya mtihani huo, ni wanafunzi 493,333 ambao ni sawa na asilimia 49.4 waliofaulu.
Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kijamii wametoa mitazamo yao kuhusihana na tatizo hili ambalo kwa uhakika linatugusa sote kama jamii moja ya Watanzania. Wapo wanaoliona tatizo la walimu kulumbana na serikali kama bomu ambalo lingelilipuka na kujidhihirisha kupitia matokeo ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Wachache hawa ndio ninaoungana nao kuamini kwamba kushuka kwa kiwango cha kufaulu kwa wanafunzi ni zao la malumbano na mivutano iliyoikumba sekta ya elimu kwa muda mrefu ikiihusisha serikali kwa upande mmoja na walimu kwa upande mwingine. Madai ya walimu dhidi ya serikali, utata wa malipo, na migomo ya mara kwa mara ni mambo ambayo yamezungumzwa kwa mapana hivyo sitayazungumzia tena hapa.

Wakati tunayatafakari haya lazima tujiandae pia kupokea bomu lingine la matokeo ya kidato cha nne ambayo yatatolewa hivi karibuni. Sitastaajabu iwapo nayo yataonyesha kushuka kwa kiwango kikubwa kama yale ya shule za msingi. Najaribu kujiuliza iwapo yule ‘mheshimiwa’ aliyewaadhibu walimu kule Bukoba kwa kuwatandika viboko kama njia mbadala ya kuwachochea katika kuongeza ufanisi wao wa kazi, ni hatua ipi angelichukua iwapo angelikuwa anadumu madarakani hadi leo. Aliitumia sababu ya kutofanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba kwa wilaya hiyo kama kigezo cha kuwasulubisha walimu hao. Sina uhakika ni jambo gain angelifanya kwa sasa na hasa kama angelikuwa na madaraka zaidi ya yale aliyokuwa nayo kwa wakati huo. Nina wasiwasi kwamba uhenda labda angeliamuru walimu hao sasa wapigwe risasi hadharani!
Labda ‘mheshimiwa’ huyo, pamoja na wale wote wliokuwa wanamuunga mkono, aliwasulubu walimu hawa kwa kufuata falsafa za Hitler tuliyemrejea mwanzoni mwa makala haya. Labda walikuwa na mawazo kama hayo huku wakirejea mafanikio yaliyofikiwa na Hitler katika miaka ya arobaini. Nina wasiwasi pia kwamba wapo wengine wengi wanaolichukulia jambo hili la kuporomoka kwa kiwango cha kufaulu kwa wanafunzi kama kushindwa kwa walimu na hivyo kuzielekeza lawama zao moja kwa moja kwa walimu hawa.
Wale wote wenye mawazo ya namna hiyo naomba kuwarudisha nyuma kidogo kwa kuwakumbusha kwamba kushindwa kufaulu kwa watoto wetu ni tatizo letu wote kama jamii ya Kitanzania. Hakuna wa kumnyooshea kidole moja kwa moja kama mhusika mkuu wa tatizo hili. Tunapoondokewa na moyo wa kizalendo tujue moja kwa moja kwamba mabo mengi yatatusibu na athari zake tutaziona kadiri
wakati unavyosonga, na hili la kuporomoka kwa matokeo ni mojawapo ya masahibu hayo.
Moyo wa kizalendo miongoni mwetu umeporomoka kwa kiwango kikubwa. Wako wapi vijana wa sasa wenye moyo kama vijana waliokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya sabini, walioomba bila mafanikio kuhairisha masomo ili kwenda vitani kule Kagera kuipigania nchi yao? Wako wapi vijana wake kwa waume wenye moyo wa kujitolea kwa nchi yao kama wale vijana waliojitolea kutoka kila pembe ya nchi na kupewa mbinu za kivita za awali wakajitoma katika uwanja wa mapambano wakati wa Vita ya Kagera? Wako wapi viongozi na maafisa wenye madaraka makubwa serikalini wenye kukubali kutumia magari ya gharama nafuu bila kushinikizwa ili gharama za kununulia magari ya anasa zielekezwe katika kuinua hali ya maisha ya mwananchi wa kawaida?
Kwa wakati huo, tunaelezwa, ilikuwa ni sifa mtu kuitumikia nchi yake, ilikuwa ni heshima kuonyesha uzalendo kwa nchi yako, ilikuwa ni fahari kuwa mwaminifu kwa jamii na nchi yako. Hayo hayafanyiki sasa, sifa kubwa ni kwa yule mwenye uwezo wa kuuibia umma. Mwenye haki anakandamizwa na mbadhirifu anapata kibali na kutukuzwa machoni pa watu. Ni nani atakubali kutenda kazi kwa moyo mmoja na kwa kujitolea akiuvumilia mshahara mdogo na hali duni wakati kila mara zinaibuliwa shutuma nzito dhidi ya watu wanaotumbua mabilioni ya shilingi ambayo ni mali ya umma?
Tukijaribu kumkumbuka Adolf Hitler tuliyemzumzia mwanzoni, sidhani kama katika Ujerumani ya enzi hizo mafisadi walikuwa na nafasi ya kutanua na kutamba huku wakiandamwa na shutuma nzitonzito za uporaji wa mabilioni. Sidhani kama walikuwepo wabunge waliokuwa wakidai kulipwa mshahara na posho unaouzidi mshahara wa mwalimu karibu mara mia moja. Sidhani kama walikuwepo wafanyakazi waliokuwa wanalipwa posho ya siku moja wawapo kwenye vikao vya bodi kiasi kinacholingana na jumla ya mishahara ya miezi mitatu ya mfanyakazi wa kawaida. Sidhani kama Hitler alikuwa na nafasi kwa watu kama hao.

Iwapo tunapenda kuiga mbinu za Hitler ni lazima turudishe moyo wa uzalendo na uwajibikaji wa pamoja. Tujue kwamba hili ni tatizo la pamoja linalotuhitaji kutimiza wajibu wetu kikamilifu na kuitendeea haki jamii iliyotupa dhamana ya kushika madaraka na kutenda kazi katika nafasi mbalimbali. Walimu wanatakiwa kuwajibika ipasavyo katika sehemu zao na kupatiwa haki zao kama inavyowastahili kulingana na hali na uwezo halisi wa kiuchumi wa serikali. Lakini pia sisi wengine tunatakiwa kutimiza wajibu wetu ipasavyo ili tusiwavunje moyo wale wanaotenda kazi katika maeneo mengine.
Ni lazima tujue na kuamini ya kwamba sisi wote tunajenga nyumba moja, hivyo tunapokusanya fito na nguzo wakatokea miongoni mwetu watu wa kuondoa fito moja moja ni lazima tuwawajibishe na kuwakemea kwa pamoja. Kushindwa kufaulu kwa watoto wetu kwa kiwango kinachostahili liwe funzo gumu kwetu tusilotakiwa kurudia. Tujifunze kutatua matatizo yetu kwa pamoja bila kuyapa nafasi malumbano huku kizazi chetu kikiteketea. Watoto hawa walioshindwa kufaulu wasipopata namna nyingine ya kusaidiwa ni mzigo wa kila mmoja wetu katika jamiii. Hakuna atakayesalimika iwapo hawa watageuka kuwa jeshi lisiloelimika.. Tutakuwa na umma usio na mwelekeeo katika siku za usoni.
Tutafakari kwa pamoja mipango ya kuwasaidia watoto hawa walioshindwa kufaulu kwa kubuni mipango ya pamoja iliyo madhubuti. Tusipojipanga vema na kuondoa tatizo hili shule zetu za sekondari zinazotutoa jasho kuzijenga kwa sasa, zitabaki kuwa mahame huku watoto wetu wakichunga mbuzi na kucheza Timpya! Tinsorola!


Johansen Kempanju
Simu: 0713 507 203
e-mail: jkempanju@yahoo.com
Mwanfunzi B.Ed Languages
Chuo Kikuu cha Tumaini Arusha











Copyright Meshack Maganga 2009
Previous
Next Post »

MAONI ConversionConversion EmoticonEmoticon