UJASIRIAMALI

Ujasiriamali ndio neno jipya. Kila mtu anaongelea habari za ujasiriamali. Pengine hii inatokana na wengi wetu kutambua kwamba nyakati zimebadilika na ujasiriamali ndio njia iliyo sahihi zaidi kama mtu anatamani mafanikio ya kweli maishani.Vijana ndio chachu zaidi ya ujasiriamali au naweza kusema ndio wanategemewa zaidi kuendeleza ujasiriamali hususani katika ulimwengu wa leo wa sayansi na tekinolojia.

Pamoja na nia nzuri walizonazo vijana, pengine ukiwemo wewe unayesoma makala hii, kipo kizingiti ambacho ni lazima watu wajifunze mbinu mpya za kukivuka. Kizingiti hicho ni aina ya elimu itolewayo mashuleni. Kwa bahati mbaya elimu zitolewazo mashuleni bado hazijawekwa katika msingi unaomuwezesha kijana kujiajiri au kwa maneno mengine kuwa mjasiriamali pindi amalizapo masomo yake.

Bado tupo katika ule mfumo wa kikoloni. Ukimaliza shule unachotakiwa ni kuanza kutafuta kazi. Zunguka jijini Dar-es-salaam kwa mfano, utakutana na vijana wengi wasomi waliohitimu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini wakiwa wamebeba vyeti vyao kwenye vijifuko vya plastiki wakizurura kusaka ajira. Hakuna anayefiria kujiajiri kwa kutumia elimu aliyoipata chuoni. Kwanini? Ndivyo ilivyo. Elimu aliyopewa haikumuandaa.Utakutana na engineer wa umeme ambaye hajawahi kubadilisha hata balbu!(nimeongeza chumvi kidogo hapa lakini kuna ukweli ndani yake!) Amesomea nadharia zaidi ya vitendo. Utakutana na mwanafunzi mhitimu wa masomo ya kilimo na mazingira ambaye hajui shamba ni nini.Hilo ni kosa katika mfumo wetu wa elimu. Ni lazima serikali ichukue jukumu la makusudi kubadili mfumo huo.

Lakini wapo wengine wengi ambao wana nia ya kweli ya kuwa wajasiriamali. Wana nia ya kujiajiri. Leo tutaangalia jinsi gani mjasiriamali chipukizi aanzishe kampeni yake. Si ushasikia kwamba biashara siku hizi ni kujuana? Ujasiriamali pia. Ni muhimu sana kujua ni nani au ni wapi uende endapo mambo yatakwama. Siongelei wapi uende kutoa au kupokea rushwa.La. Nataka kuongelea kitu kinachoitwa na wenzetu wa magharibi “networking”.Kwetu sisi hiki ndicho tunachoita “mtandao”.Mitandao ya kijamii kama vile facebook,twitter,myspace nk ni sehemu nzuri ya kutengeneza network.Itumie vizuri.

Ni muhimu kutengeneza mtandao mzuri kama unataka kuwa mjasiriamali makini na hususani kama unataka kufanikiwa. Kumbuka kwamba hapa hatuongelei kubadilishana business cards peke yake bali kumjua mtu kwa nia njema ya kusaidiana.Kumbuka neno ni “kusaidiana” na sio wewe pekee kupokea msaada.Lazima pawe na nia njema ya kusaidiana.

Kabla sijaanza kuorodhesha mbinu mbalimbali za kutengeneza ‘mtandao’ wako, naomba nikwambie kwamba siri ya kwanza ya kuanza kuwa mjasiriamali ni maandalizi.Jiandae kwa mtaji,elimu(ya darasani na mtaani),mbinu za kibiashara nk. Pili hakikisha kwamba una mapenzi ya dhati na hicho unachotaka kufanya.Usiingie kwenye biashara au ujasiriamali kwa sababu tu umemuona fulani amefanya hivyo.Kuna umuhimu mkubwa wa kujitambua katika suala zima la ujasiriamali. Baada ya kusema hivyo,sasa tuingie kwenye maeneo ya kutengeneza mtandao wako kama mjasiriamali;

Washindani wako: Biashara ni ushindani lakini sio uadui.Kama unataka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio ni vizuri sana ukawajua washindani wako wa kibiashara.Pata vipeperushi vyao,tembelea tovuti zao,wajue wateja wao na kwanini hao watu ni wateja wao.Kisha jitambulishe kwao.Najua hapa unasema;nijitambulishe?!! Ndio,jitambulishe.Kama nilivyosema ni washindani lakini sio maadui zako. Mshindani wako anaweza kukufaa pia.Anaweza kuzidiwa na kazi akakusukumia zingine.Jitambulishe,jenga uhusiano mzuri wa kibiashara.Isitoshe nyote mpo kwenye biashara moja,sekta moja.Ya kesho hamyajui.Kama kuna chama au ushirika wa watu waliomo kwenye eneo lako la ujasiriamali,jiunge.

Vyombo vya Habari: Siku hizi kuna aina nyingi zaidi za vyombo vya habari na mawasiliano. Kuna magazeti,televisheni,radio, blogs nk. Kama mjasiriamali,ni muhimu ukajuana na watu wanaoendesha au hata kumiliki vyombo hivi vya habari. Na zaidi angalia vile ambavyo vipo karibu zaidi na eneo lako la ujasiriamali.Ni rahisi zaidi kwa habari ya ujasiriamali wako kuandikwa gazetini,kuongelewa radioni,kuonekana kwenye televisheni nk kama watu wa vyombo vya habari wanajua unachofanya.Mara nyingi watu wengi wa habari wanapotaka kufanya utafiti wa jambo fulani huanza kwanza kwa kuangalia “sources” alizonazo. Kumbuka kwamba kuandikwa mara kwa mara juu ya kazi zako,ujasiriamali wako, husababisha watu kukukumbuka,kukuheshimu na hivyo kuwa rahisi kwao kufanya biashara na wewe.

Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO): Mjasiriamali makini ni yule ambaye anadhamiria kuisaidia jamii yake kwa njia moja au nyingine. Zipo faida mbalimbali za kibiashara kwa mjasiriamali ambaye hurudi nyuma na kusaidia jamii yake.Kuna faida za mapunguzo au unafuu fulani wa kodi(waulize TRA watakupa data zaidi).Isitoshe jamii iliyo bora,iwe kiafya,kielimu nk ni wateja wako wazuri wa siku za mbeleni.

Hivyo ni muhimu kujuana na watu mbalimbali wanaoendesha mashirika yasiyo ya kiserikali ama NGOs.Dhamini shughuli zao mbalimbali.Ukifanya hivyo(mara nyingi ni bei rahisi zaidi) unakuwa umesaidia jamii yako na pia umetangaza biashara yako.Lakini kuwa makini. Zipo NGO kibao siku hizi.Nyingine ni mitaji ya watu.Achana nazo.Tafuta zile ambazo ni halali na kazi wanayofanya inaonekana katika jamii.


Mwanasheria mmoja au wawili: Kama ilivyo katika maeneo mengine,msaada wa kisheria unaweza ukahitajika wakati wowote katika ujasiriamali.Unaweza kutaka ushauri,unaweza kushitakiwa nk. Ni vizuri kama ukawa unajuana na watu mbalimbali waliopo kwenye uwanja wa wanasheria. Mara nyingi watu tunaelewa mambo vizuri tunapokuwa tunaongea na watu ambao tunafahamiana nao kwa njia moja au nyingine.Wazungu wanasema unakuwa “more comfortable”. Sasa kwa sababu huwezi jua ni lini utahitaji msaada wa kisheria, ni vizuri ukajuana na mwanasheria mmoja au wawili kwa minajili ya kukusaidia endapo utaalamu wao utahitajika.

Kumbuka tu kwamba hapa siongelei msaada wa bure bali malipo fulani ingawa kutokana na kujuana huko,ni rahisi kupata punguzo la bei na pia ile faraja ya kuongea na mtu unayejuana naye.Wakati mwingine unaweza kumuuliza tu “rafiki mwanasheria” kuhusu hoja fulani ya kisheria wakati wa chakula cha mchana(lunch) na ukawa umepata jibu.Free.


Mwakilishi wako wa kisiasa: Bahati mbaya au nzuri ni kwamba hakuna biashara au ujasiriamali ambao unaweza kujitenga moja kwa moja na siasa za nchi au eneo fulani. Kuanzia kwenye ugawaji wa maeneo ya biashara, utolewaji wa leseni za biashara,sera mbalimbali za biashara nk lazima kuna ’siasa’ fulani. Sasa kwa sababu sera hizo huwa zina mkono wa siasa,ni muhimu sana kujuana na wahusika au watungaji wa sera hizo ambao mara nyingi ni wanasiasa.Ukiwajua au kujuana na wanasiasa wa eneo lako,ni rahisi kwako wewe kufikisha ujumbe,malalamiko yako na pia hisia zako katika mambo mbalimbali.Kumbuka kwamba biashara au ujasiriamali wako ni sehemu ya jamii.Ni muhimu ukamjua Balozi,Mjumbe,Mbunge,Waziri nk kutoka katika jumuiya yako au mahali ilipo biashara yako.Usije kujidanganya kwa kusema ‘ah mimi sitaki kabisa kujuana na wanasiasa”.Utakuwa unakosea na utakuwa sio mjasiriamali makini.

Kwa ufupi hayo ni maeneo ambayo ni muhimu kuyazingatia endapo “ujasiriamali” ni kitu ambacho unakitamani au tayari unakifanya. Lakini kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza katika makala zangu; fanya kazi kwa bidii na maarifa. Hiyo ndio siri ya msingi ya mafanikio katika maisha. Kujuana na watu mbalimbali muhimu peke yake haitoshi. Kazi mbele. Tukutane wiki ijayo.






Meshack Maganga 2009
Previous
Next Post »

MAONI ConversionConversion EmoticonEmoticon